Wednesday, October 10, 2012

HII NDO STORY KAMILI KUHUSU RAIS MSTAAFU ALY HASSAN MWINY ALIVYOMPELEKA KORTIN YULE DALALI ALIYEMUINGIZA MJINI KWA KULA HELA ZAKE ZA KODI

Rais Mstaafu Mwinyi amfikisha Dalali wake wa nyumba Kortin

Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi

Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, jana alipanda kizimbani kutoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jinsi alivyoibiwa zaidi ya Sh. milioni 37.

Hata hivyo, waandishi wa habari na wapiga picha, walipata wakati mgumu kutekeleza wajibu wao baada ya maofisa Usalama wa Taifa kuwadhibiti vilivyo.

Alhaj Mwinyi alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ya jinai namba 201 ya mwaka huu inayomkabili aliyekuwa mfanyakazi wake, Abdallah Mzombe, mbele ya Hakimu Mkazi, Gen Dudu.

Alhaj Mwinyi aliwasili mapema eneo la mahakama na kupelekwa moja kwa moja katika ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Illivin Mugeta, kusubiri muda wa kuanza kwa kesi kesi hiyo.

Wakati Mzee Mwinyi akiwa katika chumba cha Hakimu Mugeta, maofisa usalama walitanda katika vibaraza vinayoelekea chumba hicho na kufanya kazi ya kumhoji kila aliyepita eneo hilo.

Wale waliotaka kuingia katika chumba hicho kupata huduma, walizuiwa.

Ilipofika saa 5:00 asubuhi, walionekana askari Magereza wakipita na mshtakiwa aliyefungwa pingu mikononi wakielekea katika chumba hicho cha mahakama kwa ajili ya kuendelea na kesi hiyo.

Waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri kuingia, waliinuka na kuelekea alipopelekwa mshtakiwa huyo.

Hata hivyo, kabla ya kufikia mlangoni, maofisa usalama waliwazuia waandishi kuingia.

“Haiwahusu, haiwahusu,” alisema mmoja wa maofisa usalama hao huku mwingine akizuia waandishi kwa mikono kuingia katika chumba cha mahakama.

Kutokana na mazingira hayo, waandishi wa habari hawakuingia mahakamani na mlango wa mahakama ulifungwa, huku shahidi wa kwanza upande wa mashitaka, Alhaj Mwinyi, akitoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali, Charles Anindo.

Alhaj Mwinyi alimaliza kutoa ushahidi saa 7:00  mchana na kutolewa kwa kupitia mlango wa nyuma na kupanda katika gari aina ya Toyota Land Cruiser maarufu kama `shangingi' lenye namba za usajili T914 BJT, lililokuwa likimsubiri.

Mzee Mwinyi alitoa ushahidi katika kesi ya kutapeliwa zaidi ya Sh. milioni 37 na mfanyakazi aliyemwamini kukusanya kodi katika nyumba mbili tofauti zilizopo jijini Dar es Salaam.

Katika hati ya mashitaka, inadaiwa kwamba kati ya Januari, 2011 na Julai, 2012, maeneo ya Mikocheni, Dar es Salaam, Abdallah Mzombe, akiwa mfanyakazi wa Rais mstaafu Mwinyi, aliiba Sh. 17,640,000 alizokusanya kodi katika nyumba namba 481 Kitalu `A'  eneo la Mikocheni kwa ajili ya kodi mwaka 2011/2012 na 2012/2013 alizotakiwa kuzikifikisha kwa Rais huyo mstaafu, lakini hakufanya hivyo.

Mshtakiwa pia anadaiwa katika kipindi hicho maeneo ya Msasani Village, aliiba Sh. 19,800,000 alizokusanya kodi katika nyumba namba 55 Block `C' Msasani Village kwa ajili ya mwaka 2011/2012 na 2012/2013.

Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashitaka hayo na  yuko rumande baada ya kukosa dhamana.
Hii ni mara ya pili kwa Rais mstaafu nchini kwenda mahakamani kutoa ushahidi.

Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Mei 7, mwaka huu alisimama kizimbani katika Mahakama ya kisutu kutoa ushahidi akiwa shahidi wa Jamhuri akimtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.

Mkapa alimtetea Profesa Mahalu na aliyekuwa Afisa Mwandamizi katika ubalozi huo, Grace Martin ambao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kuisababishia serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi huo.

Mkapa aliwatetea Profesa Mahamu na Grace kwamba walikuwa na baraka zote za serikali na baadaye Mahakama hiyo iliwaachia huru.

No comments:

Post a Comment