Wednesday, October 17, 2012

HIKI NDO KILICHOSABABISHA KIFO CHA YULE KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA MWANZA

YADAIWA NI KISASI CHA
MAPENZI, MTUHUMIWA
ATIWA MBARONI, DK BILAL
AONGOZA WAOMBOLEZAJI
DAR
Waandishi Wetu MWELEKEO wa upelelezi wa mauaji ya aliyekuwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow umebadilika na sasa tukio hilo linahusishwa na kisasi cha mapenzi na tayari mtu mmoja anayedaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi Mwalimu Dorothy Moses kutiwa mbaroni na
polisi.Awali, ilidaiwa kwamba Kamanda Barlow ambaye aliuawa kwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi muda mfupi baada ya kumfikisha mwalimu huyo nyumbani kwake, alivamiwa
na majambazi.
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI, Robert Manumba alithibitisha jana kukamatwa kwa mtu huyo (jina tulihifadhi) akisema: "Ni kweli mtu mmoja
amekamatwa, lakini kwa
sasa siwezi kuzungumzia
kwa kina kuhusu suala hilo kwa sababu bado tunamhoji na tunaendelea na uchunguzi.
Tutakapokamilisha, tutatoa
taarifa." Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola pia alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo. Hata hivyo, alisema
amesikia habari hizo kwa kuwa yuko safarini kwenda mkoani Kilimanjaro kwenye mazishi ya kamanda huyo...
"Hayo nimesikia, lakini kwa sasa sipo Mwanza hivyo siwezi kuzungumzia lolote."
Habari za uhakika kutoka ndani ya
Jeshi la Polisi, zinaeleza kwamba
upelelezi wa mauaji hayo
umefanikiwa kwa hatua kubwa na
kwamba mtu huyo alikamatwa Dar es Salaam baada ya kuwekewa mtego na makachero waliopo katika timu ya
uchunguzi na alisafirishwa hadi
Mwanza ambako anashikiliwa na jeshi hilo.
Ilielezwa kuwa mtu huyo alikamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa za siri za kiitelejensia kutoka kwa watu mbalimbali.
"Kuna hali imefunguka na imesaidia sana. Inaonyesha kwamba Dorothy alikuwa na uhusiano na mtu huyu ambaye alikuwa akifika nyumbani
kwake, kama mumewe na watu
wanajua jambo hili," alieleza mmoja wa askari polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Alisema kwamba uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba uamuzi wa mwalimu huyo kusitisha uhusiano wa mapenzi na mtu huyo huenda ndicho
chanzo cha mauaji hayo lengo likiwa ni kumshawishi Dorothy kurejesha uhusiano.
"Mimi natambua kwamba huyu jamaa na Dorothy walikuwa na uhusiano na inajulikana mjini kuwa hata mke wa mtuhumiwa anatambua jambo hilo
kwani walishagombana siku moja
mjini na hata katika msiba nyumbani kwao na mtuhumiwa," alisema mama mmoja (jina tunalo), aliyejitambulisha
kama mmoja wa marafiki wa karibu wa Dorothy.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitangiri (jina tunalo), anasema amekuwa akimfahamu mtuhumiwa aliyekamatwa kama baba mwenye nyumba hiyo na kila mara amekuwa akimkuta hapo nyumbani wakati wa
kujisomea na wanafunzi wenzake.
"Mimi ninamfahamu kama baba wa rafiki yangu na nimewahi kumkuta wakati wa kujisomea hapo nyumbani na watoto wa nyumba hiyo."
Dorothy ambaye ametajwa kuwa
mjane, ni Mwalimu katika Shule ya
Msingi Nyamagana na tangu kufariki
kwa mumewe Ofisa wa zamani wa
TRA, Modest Lyimo mwaka 1997.
"Watu wote wanajua kwamba
mtuhumiwa alikuwa akitembea na
huyo mwalimu, wameonekana mara
nyingi wakiwa muziki," alieleza mmoja
wa ndugu wa karibu wa mke wa
mtuhumiwa.
Hili ni tukio la tatu mkoani Mwanza
kutokea kwa ofisa wa polisi kuuawa.
Katika tukio la awali lililotokea mwaka
1987, askari aliyetambulika kwa jina la
Inspekta Gamba aliuawa kwa risasi na
watu wanaosadikiwa kuwa ni
majambazi eneo la Nyakato na katika
tukio la pili mwaka 1997, aliyekuwa
Mkuu wa Kituo cha Kati ASP Mahende
aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la
Bugando saa nne usiku alipokuwa
akifuatilia majambazi waliokuwa
wakijitayarisha kuvamia.
Dar wamuaga Kamanda Barlow
Makamu wa Rais, Dk Mohamed
Gharib Bilal aliongoza waombolezaji
waliofika kutoa heshima za mwisho
kwa mwili wa marehemu Barlow
nyumbani kwake, Ukonga Dar es
Salaam jana.
Mwili wa Kamanda Barlow ambao
unasafirishwa leo kwenda mkoani
Kilimanjaro kwa mazishi, uliwasili
nyumbani kwake saa 6.45 kabla ya
kupelekwa katika Kanisa  la Mtakatifu
Agustino, Ukonga kwa ajili ya ibada na
kutoa heshima za mwisho.
Akitoa salamu za Serikali, Naibu Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira
Silima alisema kifo cha Kamanda
Barlow ni pengo kwa taifa...
"Tutahakikisha watuhumiwa
wanapatikana kwa mikono yote miwili
na hatua za kisheria zinachukuliwa
dhidi yao."
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said
Mwema alisema juhudi za kuwasaka
watuhumiwa zinaendelea kwa
ushirikianao wa wananchi.
"Kifo cha Kamanda Barlow kimeacha
pengo kwani hivi sasa askari mmoja
analinda watu 1,300 hivyo kwa kifo
chake unaweza kuona ni pengo la
aina gani na ukilinganisha yeye
alikuwa kamanda wa mkoa mzima,"
alisema IGP Mwema.
Alisema jeshi lake litaendelea kulinda
amani ya wananchi na kifo cha
Kamanda Barlow kinalifanya liongeze
nguvu.
Akitoa mahubiri, Padri Veri Urio
alisema kila jambo hutokea kwa wakati
na kifo cha Kamanda Barlow
kimesababishwa na watu. Alisema
mwenye mamlaka ya kuondoa uhai
wa mtu ni Mungu pekee hivyo
waliosababisha kifo chake siku ikifika,
watajibu kwa nini walifanya hivyo.
IGP Mstaafu, Omary Mahita alisema
atamkumbuka Kamanda Barlow kwa
uchapaji wake kazi tangu akiwa polisi
Interpol (polisi kimataifa)alifanya kazi
kwa weledi uliotukuka.
"Daima nitamkumbuka kwani
nimefanya naye kazi sehemu tofauti
na askari waliobaki waige mfano wake
wa uwajibikaji" alisema Mahita.
Mbali ya Dk Bilal, viongozi wengine
walioshiriki katika ibada hiyo jana ni
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Said Meck Sadiki, makamanda wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
makamanda wa polisi, viongozi  wa
Serikali na vyama vya siasa na
wananchi.

No comments:

Post a Comment